Mwenyekiti wa CUF Prof. Ibrahim Lipumba akiwahutubia maelefu ya wanachama na wapenzi wa Chama hicho katika viwanja vya Muembe Yanga Wilaya ya Temeke jijini Dar es Salaam ambako kulifanyika mkutano wa hadhara.
Katibu Mkuu wa CUF Maalim Seif Sharif Hamad akimkaribisha Mwenyekiti wa Chama hicho Prof. Ibrahim Lipumba katika viwanja vya Muembe Yanga Wilaya ya Temeke jijini Dar es Salaam ambako kulifanyika mkutano wa hadhara wa Chama hicho. Katikati ni Makamu Mwenyekiti Mhe. Machano Khamis Ali.
Wafuasi wa CUF waliopata ajali siku ya mapokezi ya Prof. Lipumba tarehe 11/03/2012, wakiwasili katika viwanja vya Muembe Yanga Temeke Dar es Salaam kwa ajili ya kumuona na kumsikiliza Mwenyekiti huyo wa CUF Prof. Ibrahim Lipumba.Picha na Salmin Said-Ofisi Ya Makamu Wa Kwanza Wa Rais Zanzibar
---
Mwenyekiti wa Chama Cha Wananchi CUF Prof. Ibrahim Lipumba amewataka watanzania kusimama imara na kujipanga katika kutoa maoni ya katiba mpya, ili kuhakikisha kuwa katiba inaweka wazi suala la maliasili kuwa rasilimali za Watanzania.
Amesema Tanzania imebarikiwa kuwa na maliasili nyingi zikiwemo dhahabu, almasi, Tanzanite, copper na madini mengine kadhaa, lakini bado rasilimali hizo hazijawanufaisha wananchi kutokana na kutokuwepo utaratibu unaoeleweka juu ya mgawano wa rasilimali hizo.
Akizungumza katika mkutano wa hadhara wa Chama hicho wenye lengo la kuwashukuru wananchama na wakaazi wa Dar es Salaam pamoja na Mikoa jirani kutokana na kujitokeza kwa wingi kwenye mapokezi yake tarehe 11/03/2012 Prof. Lipumba amesema iwapo kutawekwa utaratibu maalum kikatiba, maliasili hizo zinaweza kuwanufaisha Watanzania wote.
Katika mkutano huo uliofanyika viwanja vya Muembe Yanga Wilaya ya Temeke jijini Dar es Salaam, Prof. Lipumba amewapongeza wanachama na wananchi waliojitokeza kwenye mapokezi hayo, na kutaka moyo waliounyesha kwake siku hiyo uendelezwe katika kukijenga chama hicho na kuwa dira ya uchaguzi mkuu ujao.
Prof. Lipumba amefahamisha kuwa kutokana na kutokuwepo kwa mipango imara ya kiuchumi nchini, kumepelekea kuwepo kwa mfumko mkubwa wa bei kwa zaidia ya asilimia 50, jambo ambalo linadumaza maendeleo ya Watanzania waliopata uhuru miaka 50 iliyopita.
Amesema kipindi cha miaka 50 ni kikubwa kuweza kuleta mapinduzi ya kweli yw kiuchumi na maendeleo endelevu, na kwamba nchi nyingi tayari zimefanikiwa zikiwemo Singapore, Malaysia na Korea ya Kusini.
“Tunahitaji uongozi wenye dira ya kuikomboa Tanzania kiuchumi, nchi yetu ina utajiri mkubwa lakini hakuna mipango imara kutokana na ombwe ya uongozi uliopo”, alisema Prof. Lipumba ambaye alirejea nchini mapema mwezi huu kutoka Marekani alikokuwa alifanya utafiti kuhusu mambo ya demokrasia na maendeleo ya kiuchumi.
Amewaeleza maelfu ya wanachama na wapenzi wa Chama hicho kuwa tayari amepata mwaliko mwengine wa kwenda nchini Barcelona mwishoni mwa mwezi huu, ambako atakutana na wataalamu wawili wa kuchumi kutoa nchi za Urusi na Ubelgiji kwa lengo la kujadili matatizo ya kisiasa ya nchi za kiarabu na athari za kiuchumi na kisiasa zinazoweza kujitokeza kwa nchi nyengine.
Mapema Katibu Mkuu wa Chama hicho Maalim Seif Sharif Hamad amepongeza mapokezi makubwa aliyopewa Prof. Lipumba ambayo amesema yanathibitisha kuwa CUF kweli ni Chama Cha Wananchi, sambamba na wanachama kuwa na uchungu na Chama chao.
Maalim Seif amekebehi kwa wale wanaodai kuwa CUF ni CCM ‘B’ kwamba wana wivu wa kisiasa, na kutoa wito kwa wanachama kutokubali kuyumbishwa katika kukiendeleza chama hicho.
Katika hatua nyengine mjumbe wa baraza kuu la uongozi la Chama hicho aliyepewa onyo kali wakati Mwakilishi wa Jimbo la Wawi Mhe. Hamad Rashid Mohd pamoja na wenzake walipofukuzwa uanachama Bw. Yassir Mrotwa, ameibuka na kuomba radhi kutokana kukifikisha Chama hicho mahakamani.
Amesema atafuatilia mwenendo wa kesi hiyo ili kufuta saini yake isitumike kwenye mwendelezo wa kesi hiyo.
Wakati huo aliyekuwa naibu mkurugenzi wa uchaguzi wa CUF taifa Bw. Khamis Katuga ambaye alikihama chama hicho na kuhamia CCM, amerejea tena CUF ambapo amerejesha kadi ya CCM na kukabidhiwa kadi ya CUF.
Ametahadharisha kuwa tatizo kubwa linalorejesha nyuma maendeleo ya chama hicho ni kutokanyika kwa vikao katika ngazi ngazi mbali mbali, huku akieleza sababu zilizomrejesha tena CUF kuwa ni uimara na sera zinazotekelezeka za chama hicho, huku akifunga maelezo yake kwa usemi “asiyejua kufa achungulie kaburi”.
Na
Hassan Hamad
Ofisi Ya Makamu Wa Kwanza Wa Rais Zanzibar
0 comments:
Post a Comment