Na Ripota wetu, jijini Dar .
KISURA wa Tanzania 2011, Lethina Christopher, amejitosa katika kuhamasisha wanawake kujifunza na kuuelewa ugongwa wa saratani ya matiti akishirikiana na Asasi ya Saratani ya Matiti Tanzania (TBCF).
TBCF, chama cha hiari kisicho cha kiserikali na cha kujitegemea, kilianzishwa na wanawake jasiri ambao wamegundulika kuwa na ugonjwa huo pamoja na wanawake wachache wa kujitolea.
Akizungumza na waandishi wa habari katika hoteli ya Southern Sun, Dar es Salaam jana, Lethina alisema kuwa ameamua kushirikiana na TBCF kutokana na kuguswa kwake na ugonjwa huo ambao si tu unawaathiri wanawake, bali pia familia zao, hasa watoto wadogo pindi wanapopoteza wazazi wao.
“Kwa ushirikiano na TBCF, nitahamasisha wanawake wa Tanzania, wasichana kwa wazee kuchunguza matiti yao kila mara ili wakijua kama wana dalili za ugonjwa huo, wawahi kupata tiba hospitalini kabla ya tatizo hilo kuwa kubwa,” alisema Lethina.
Awali, mwanzilishi wa TBCF, Angela Kuzilwa ambaye aligundulika kuwa na saratani ya matiti mwaka 2004, alisema kuwa lengo la taasisi yao hiyo ni kutoa hamasa kwa wanawake waweze kuelewa na kuufahamu vizuri ugonjwa huo ili pindi watakapogundulika, waweze kwenda hospitali mapema na kuwahi kupata matibabu kwani saratani ya matiti ikigundulika mapema, hutibika.
Alisema kuwa saratani ya matiti ni mojawapo ya magonjwa hatari yanayowapata wanawake wengi Tanzania ingawa inasemekana saratani ya kwanza ni ya shingo ya kizazi na kwamba wanawake wengi waliogundulika na ugonjwa huo, wanakumbana na matatizo mengi, huku matibabu yake yakiwa ni ghali mno.
“Saratani ya aina yoyote inahusishwa na kifo kwani hata mimi nilipoambiwa, nilijua siku za maisha yangu ni fupi. Nimepata upasuaji wa kuondolewa titi na kufanyiwa matibabu na leo ninaishi kwa matumaini nikifahamu kuwa kila mtu ana siku yake ya kufa,” alisema.
Alisema kuwa katika kuhakikisha jamii ya Watanzania inakuwa na ufahamu wa kutosha kuhusiana na ugonjwa huo, wameandaa matembezi ya hisani yatakayofanyika Jumapili ambapo yataanza saa 1:30 asubuhi na kumalizikia viwanja vya Mnazi Mmoja, jijini.
Aliwataka wenye nia ya kushiriki matembezi hayo kujiandikisha katika vituo vya Mlimani City, Milleum Towers, Shoppers Plaza na Woolworth kuanzia saa 12:00 mpaka saa 1:00 asubuhi.
Angela alisema kuwa wameamua kufanya matembezi hayo siku hiyo kwa sababu Oktoba huwa ni Mwezi wa Ufahamu wa Saratani ya Matiti Duniani.
Juu ya kazi za asasi yao, alisema huwa wanatoa msaada kwa wanawake waliogundulika na saratani ya matiti kwa kutoa matiti bandia na sidiria maalum, kuwatembelea wagonjwa hospitali na majumbani na kutoa msaada wa fedha na chakula, kuitisha vikao vya wanawake waliogundulika na saratani ili kubadilishana mawazo na kisikia changamoto wanazokumbana nazo, ikiwa ni pamoja na kutoa ushauri nasaha kutokana na matibabu na matatizo yake.
“Asasi yetu kwa mwezi huu pia imeandaa Chakula cha Usiku tarehe 28 Oktoba 2011 kuchangia mfuko wa Asasi hii ili kuweza kufikisha malengo yake ya kuweza kueneza ufahamu na elimu ya saratani ya matiti kwa jamii ya Kitanzania.”
Alitoa shukurani kwa mashirika na asasi mbali mbali ambazo zimejitolea kufanikisha matembezi hayo ya Jumapili ambazo ni Shirika la Susan G. Komen for the Cure kutoka United States of America, Foundation for Civil Society, Twiga Cement, Shear Illusions, PPF, Beautiful Tanzanie Agency (BTA) ambao ndio waratibu wa shindano la Kisura wa Tanzania na Hoteli ya Southern Sun.
0 comments:
Post a Comment